Wanafunzi wasichana wa Hawzat Ummul-Banin (a.s.) iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam, wamefanya zoezi la usafi wa mazingira kwa lengo la kuadhimisha kumbukumbu ya Imam Hussein (a.s.) na kuendeleza ujumbe wa Karbala wa marekebisho ya jamii, maadili mema na huduma kwa jamii.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s.) –ABNA–, wanafunzi wasichana wa Hawzat Ummul-Banin (a.s.) iliyopo Kigamboni, Jijini Dar es Salaam, wamefanya zoezi la usafi wa mazingira wakiongozwa na Mudir wa Hawza, Sheikh Eid Wambua, akisaidiwa na Sheikh Anuari Mputa pamoja na Ukhti Asma Sulaiman.
Zoezi hilo limefanyika katika kuadhimisha kumbukumbu ya Sayyid wa Mashahidi, Imam Hussein (a.s.), mjukuu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), aliyeuawa kwa dhulma katika ardhi ya Karbala.
Washiriki wa shughuli hiyo wameeleza kuwa usafi wa mazingira ni sehemu ya kutekeleza mafundisho ya Kiislamu na kuendeleza ujumbe wa Karbala, kwani mapinduzi ya Imam Hussein (a.s.) yalilenga kuurekebisha Umma na kuurejesha katika njia sahihi ya Uislamu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.).
Aidha, imeelezwa kuwa Uislamu unatoa umuhimu mkubwa kwa usafi, kwa kuwa usafi ni sehemu ya imani na ni miongoni mwa maadili ambayo Imam Hussein (a.s.) alipigania kuyahuisha katika jamii.
Imam Hussein (a.s.) amesema:
"Hakika nimetoka kwa ajili ya kutafuta marekebisho katika Umma wa babu yangu. Ninataka kuamrisha mema na kukataza maovu, na kufuata mwenendo wa babu yangu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) na wa baba yangu Ali bin Abi Talib (a.s.)."
Kwa mujibu wa waandaaji wa shughuli hiyo, zoezi la usafi wa mazingira ni njia ya kuonesha kwa vitendo mafunzo ya Karbala kwa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usafi, huduma kwa jamii na kuishi kwa kuzingatia maadili ya Kiislamu.
Your Comment